Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Kwenye siasa, baada ya uchaguzi, wanasiasa hutumia kauli ya “tuweke uchama pembeni, tuitangulize nchi mbele.” Kauli hiyo ina maana kubwa pia katika soka la Tanzania, hususan wakati klabu zetu zinaposhiriki michuano ya kimataifa.
Kuishabikia Simba SC katika michuano ya kimataifa wakati wewe ni shabiki wa Yanga SC si dhambi, kwa sababu katika hatua hiyo klabu hiyo inawakilisha Tanzania. Vivyo hivyo, shabiki wa Simba anapoiunga mkono Yanga katika mashindano ya Afrika, haivunji sheria wala kupoteza uaminifu kwa klabu yake, bali anashiriki kuipeperusha bendera ya Taifa.
Pongezi kwa mashabiki waliojitokeza kwa kuiunga mkono Azam FC katika mchezo wake dhidi ya Zed FC ya Misri, ambapo Azam ilishinda bao 1-0 na kufuzu kwa jumla ya mabao 2-1 katika michezo miwili. Pongezi pia kwa mashabiki waliojitokeza kuiunga mkono Singida Black Stars, ambayo imeiondosha Tusker FC ya Kenya kwa Jumla ya mabao 2-1 katika michuano hiyo,na zote kwa pamoja kutinga hatua ya makundi kombe la shirikisho barani Afrika
Ushiriki wa mashabiki katika michezo hiyo unaonyesha kuwa soka lina nafasi ya kuwaunganisha Watanzania bila kujali tofauti za klabu wanazozishabikia katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Azam FC na Singida Black Stars ni miongoni mwa klabu ambazo hazina idadi kubwa ya mashabiki kwa kulinganisha Simba na Yanga, hata hivyo, hilo halipunguzi umuhimu wa safari zao katika michuano ya kimataifa. Kadiri zinavyoendelea kusonga mbele, ndivyo zinavyohitaji kuuungwa mkono kutoka kwa mashabiki wa klabu nyingine ili kuongeza nguvu ya uwakilishi wa Tanzania katika soka la Afrika.
Kwa mantiki hiyo, kuanzia hatua za awali za michuano ya kimataifa, ni wajibu wa mashabiki kuweka tofauti za ushindani wa ndani pembeni na kuungana kuziunga mkono timu zinazoiwakilisha nchi, Ushindani wa Simba na Yanga unaweza kuendelea katika ligi ya ndani, lakini inapofika kwenye michuano ya Afrika, jambo la msingi linapaswa kuwa mafanikio ya klabu za Tanzania.
Klabu zinapofanya vizuri kimataifa, zinaongeza nafasi ya Tanzania kuwa na uwakilishi mkubwa katika mashindano ya Afrika na kulipa soka letu nafasi ya kuendelea kukua, hivyo, sapoti ya mashabiki si suala la kujaza uwanja pekee, bali pia ni sehemu ya kuonyesha mshikamano na uzalendo.
Kwa kutambua nafasi ya mashabiki katika soka, kila mmoja ana wajibu wa kuziunga mkono timu zetu zinapokuwa kwenye jukumu la kuiwakilisha nchi. Hata wahenga walisema, “shughuli ni watu na watu ni sisi.”
Ikumbukwe kuwa kwenye timu 32 kutoka barani Afrika , Tanzania imetoka timu nne kushiriki hatua ya makundi klabu bingwa na shirikisho. Simba Sc , Yanga Sc, Azam Fc na Singida black stars , ni majeshi ambayo yamesimama kwaajili ya kuhakikisha kikombe Cha Afrika kinakuja Tanzania , hivyo ni wajibu wa Kila mmoja kufunga mkanda wa uzalendo na kuwaunga mkono wanajeshi wetu kuhakikisha wanashinda vita hiyo.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment