Simba kukata kiu ya ubingwa 2026/27


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kwa misimu mitano sasa, klabu ya Simba SC imeshindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku watani wao wa jadi, Yanga SC, wakitawala mashindano hayo kwa kipindi hicho chote.

Hata hivyo, huenda msimu wa 2026/27 ukawa tofauti kwa Simba baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Yanga, na kuanza kusahihisha makosa ambayo katika misimu miwili iliyopita yaliigharimu katika mbio za ubingwa.

Katika misimu ya 2024/25 na 2025/26, Simba ilikosa taji kwa tofauti ndogo ya alama, huku matokeo ya michezo dhidi ya Yanga yakiwa miongoni mwa mambo yanayoweza kuangaliwa katika kuelewa namna mbio hizo zilivyoamuliwa.

Msimu wa 2024/25, Simba ilimaliza ligi ikiwa na alama 78, huku Yanga ikitwaa ubingwa kwa alama 82, tofauti ya alama nne, Katika michezo miwili ya watani hao, Simba ilifungwa bao 1-0 katika mzunguko wa kwanza na mabao 2-0 katika mzunguko wa pili, hivyo kupoteza jumla ya alama sita.

Matokeo hayo yanaacha nafasi ya kujiuliza kuwa Simba ingeweza kutwaa ubingwa iwapo ingepata matokeo tofauti katika michezo hiyo, ingawa mbio za ligi huamuliwa na matokeo ya michezo yote ya msimu.


Msimu wa 2025/26, tofauti ilikuwa ndogo zaidi, Simba ilimaliza ikiwa na alama 73, huku Yanga ikitwaa ubingwa kwa alama 75. Tofauti na msimu uliotangulia, michezo miwili ya watani hao iliisha kwa sare ya 0-0 na 2-2, kila timu ikipata alama mbili katika michezo hiyo.

Sasa, katika msimu wa 2026/27, Simba imeanza kuonyesha dalili za kurekebisha sehemu hiyo baada ya kuifunga Yanga mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ushindi ulioipa alama tatu na kuipandisha kileleni mwa msimamo wa ligi.

Ushindi huo una umuhimu katika mbio za ubingwa kwa sababu unaipa Simba faida ya alama dhidi ya mpinzani wake wa karibu, tofauti na misimu iliyopita ambayo matokeo ya michezo yao yalikuwa sehemu ya mjadala kuhusu namna ubingwa ulivyoamuliwa.

Hata hivyo, kukata kiu ya ubingwa bado ni uwezekano, si uhalisia kwani Soka huamuliwa ndani ya dakika 90 za kila mchezo, na ubingwa hupatikana kwa matokeo ya msimu mzima, si kwa ushindi dhidi ya mpinzani mmoja pekee.

Pamoja na hilo, historia ya misimu ya hivi karibuni inaonyesha namna michezo ya Simba na Yanga inavyoweza kuwa na nafasi katika mbio za ubingwa. Kwa hiyo, ushindi wa Simba msimu huu unaweza kuwa mwanzo wa safari ya kurejesha taji Msimbazi, iwapo itaendeleza matokeo hayo katika michezo inayofuata.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments