Hili hapa suluhisho la kurudisha mvuto wa Dabi ya Kariakoo


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kwa miaka mingi, Dabi ya Kariakoo imekuwa ikivuta hisia za mashabiki wa soka nchini kutokana na maandalizi, tambo na hamasa zinazoambatana na mchezo huo. Mashabiki kutoka mikoa mbalimbali wamekuwa wakisafiri kwenda uwanjani kushuhudia timu zao zikichuana, huku utani wa mashabiki ukichangia kuongeza hamasa kabla ya mchezo.

Simba na Yanga pia ni sehemu kubwa ya taswira ya soka la Tanzania kimataifa. Kwa kiasi kikubwa, namna timu hizi zinavyojiandaa, zinavyoshindana na zinavyovutia mashabiki huchangia jinsi soka la Tanzania linavyoonekana nje ya mipaka ya nchi.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, hamasa inayotangulia Dabi ya Kariakoo imeonekana kupungua ambapo tambo, utani na shughuli za kutangaza mchezo huo hazijawa na mwendelezo uliokuwa ukionekana katika vipindi vilivyopita ambapo moja ya mambo yanayoweza kujadiliwa katika kurejesha hali hiyo ni mfumo wa mapato ya mchezo.

Kwa utaratibu ambao timu mwenyeji hupata mapato yote ya mlangoni, timu inayokuwa mgeni haina sehemu ya moja kwa moja ya mapato hayo. Hali hii inaweza kupunguza motisha ya timu zote mbili kushiriki kwa kiwango sawa katika shughuli za kuhamasisha mashabiki, hasa pale zinapoona kuwa juhudi za kutangaza mchezo zinaweza kuongeza mapato ya mpinzani.

Suluhisho linaweza kuwa kupitia mazungumzo kati ya Bodi ya Ligi, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) , Simba pamoja na Yanga ili kutathmini uwezekano wa kuweka utaratibu maalumu wa kugawana mapato ya mlangoni katika dabi hiyo.

Kwa mfano, mapato hayo yanaweza kugawanywa kwa uwiano wa asilimia 50 kwa kila timu, baada ya kuzingatia gharama na taratibu zitakazokubaliwa, mfumo huo unaweza kuzipa klabu zote mbili sababu ya kushiriki kikamilifu katika kampeni za kuitangaza dabi, kuhamasisha mashabiki na kuongeza idadi ya watazamaji wanaofika uwanjani.

Hata hivyo, kugawana mapato pekee hakutoshi pia Bodi ya Ligi na TFF zinapaswa kukutana na viongozi wa Simba na Yanga ili kuweka mkakati wa pamoja wa kuitangaza dabi, kuandaa shughuli za mashabiki na kuhakikisha ushindani wao unaendelea kuwa sehemu ya kukuza soka la Tanzania.

Ni muhimu pia klabu hizo kutofautisha utani unaojenga hamasa na vitendo vinavyoweza kuathiri uhusiano wa mashabiki au usalama wa mchezo, Lengo linapaswa kuwa kuendeleza ushindani ndani ya uwanja na kuongeza hamasa nje ya uwanja bila kuathiri misingi ya mchezo huo.


Dabi ya Kariakoo ni zaidi ya dakika 90 za mchezo, ni sehemu ya utamaduni wa soka la Tanzania na fursa ya kuonyesha uwezo wa klabu zetu kuvutia mashabiki na kujenga thamani ya ligi na mchezo.

Kwa hiyo, marekebisho ya mfumo wa mapato na ushirikiano kati ya wadau yanaweza kuwa hatua ya kuanzia katika kurejesha hamasa ya dabi hiyo. Simba na Yanga zikipewa nafasi ya kuona manufaa ya pamoja katika mchezo wao, zinaweza kuongeza juhudi za kuifanya Dabi ya Kariakoo iendelee kuvutia mashabiki nchini na nje ya mipaka ya Tanzania.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments