TIMU ZA AFRIKA NA MATUMAINI YA KUFUZU HATUA INAYOFUATA KOMBE LA DUNIA

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Mzunguko wa kwanza hatua ya makundi katika Kombe la Dunia 2026 umekamilika kwa timu zote, huku wawakilishi wa Afrika wakionyesha dalili za kuweza kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Kati ya timu 10 zinazoiwakilisha Afrika, sita zimefanikiwa kuvuna alama katika michezo yao ya kwanza, hatua inayoziweka katika nafasi ya kuendelea kupambania kufuzu hatua ya mtoano.

Kwa upande wa timu za Ivory Coast na Ghana ndizo timu zilizopata matokeo bora zaidi baada ya kuanza kampeni zao kwa ushindi na kujikusanyia alama tatu kila moja, matokeo yanayozisogeza karibu na hatua inayofuata.

Mbali na ushindi , timu za Morocco, Misri, Cape Verde na Congo zimepata sare katika michezo Yao ya ufunguzi na kuvuna alama moja kila moja.

Hata hivyo, Afrika Kusini, Tunisia, Algeria na Senegal zilianza mashindano kwa kupoteza michezo yao ya  kwanza na kubaki bila alama.


Kwa matokeo hayo, asilimia 60 ya timu za Afrika zimefanikiwa kupata angalau alama moja baada ya mzunguko wa kwanza wa hatua ya makundi, jambo linalotoa matumaini kwa bara hilo kuelekea michezo inayofuata.

Wakati mzunguko wa pili wa hatua ya makundi ukianza Juni 18, 2026, timu zilizovuna alama zitakuwa zikisaka kuimarisha nafasi zao za kufuzu, huku zile zilizopoteza zikihitaji matokeo chanya ili kurejesha matumaini ya kusonga mbele katika mashindano hayo.

Matokeo ya mzunguko huo wa pili yanatarajiwa kutoa picha halisi ya nafasi za timu za Afrika katika harakati za kufuzu hatua ya 32  bora ya Kombe la Dunia 2026.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.

0/Post a Comment/Comments