✍️ Rashid Msiri
Mwanakwetu Blog
Kuna wachezaji ambao hucheza mpira kwa ajili ya dakika 90 tu, lakini kuna wengine ambao hucheza na kuacha alama isiyofutika mioyoni mwa mashabiki milele. Patrick Mutesa Mafisango alikuwa mmoja wa nyota wa aina hiyo — kiungo mwenye kipaji cha kipekee, moyo wa kipekee na uwezo mkubwa wa kuifanya Simba SC icheze kwa utulivu, ubunifu na hadhi kubwa kila alipokanyaga dimbani.
Nani asiyeikumbuka simba iliyojaa mafundi wa kabumbu kama vile Haruna Moshi Boban, Emmanuel Okwi,Amri Kiemba na wengine wengi lakini jina la Patrick Mutesa Mafisango lilisikika mitaa yote ya msimbazi na viunga vyake.
Alikuwa si tu mchezaji wa mpira, bali alikuwa “maestro” wa kweli wa eneo la kiungo. Kila alipogusa mpira, mashabiki waliinuka majukwaani wakiamini kuna jambo zuri linaenda kutokea. Utulivu wake akiwa na mpira, pasi zake zenye macho, mapambano yake uwanjani na moyo wake wa kujituma vilifanya jina lake kuwa sehemu ya historia ya Simba Sports Club na soka la Tanzania kwa ujumla.
Patrick Mafisango alikuwa aina ya wachezaji wanaocheza kwa akili, nidhamu na mapenzi ya kweli kwa timu. Hakupenda makelele, lakini miguu yake ilizungumza kwa lugha ambayo mashabiki waliielewa vizuri sana. Alikuwa kiungo aliyekuwa na uwezo wa kuunganisha safu zote za timu, kuamsha morali ya wenzake na kuwapa matumaini mashabiki kila mchezo ulipoonekana kuwa mgumu.
Ndani ya uwanja alikuwa mpiganaji, lakini nje ya uwanja alikuwa mtu mwenye heshima, unyenyekevu na upendo mkubwa kwa watu waliomzunguka. Hilo ndilo lililofanya kifo chake kuwa pigo kubwa sana kwa mashabiki, wachezaji na familia nzima ya soka Afrika Mashariki. Habari za kifo chake zilipoenea, machozi, simanzi na majonzi vilitawala mioyo ya wengi waliowahi kushuhudia kipaji chake kikubwa.
siku kama ya leo, jina la Patrick Mutesa Mafisango bado linaishi kwenye nyoyo za mashabiki wa Simba SC. Miaka inaweza kupita, vizazi vinaweza kubadilika, lakini kumbukumbu ya maestro huyo itaendelea kubaki hai kama ishara ya uzalendo, kipaji na mapenzi ya kweli kwa mchezo wa soka.
Wapo wachezaji wengi waliopita Simba SC, lakini wachache sana walioweza kuacha hisia, heshima na kumbukumbu nzito kama alizoacha Patrick Mafisango. Aliondoka duniani mapema, lakini urithi wake umeendelea kuzungumza kupitia historia, kupitia mashabiki, na kupitia kila anayelitaja jina lake kwa heshima kubwa.
Legends never die… Mafisango Maestro ataendelea kuishi kwenye historia ya Simba SC.”
✍️ Rashid Msiri
Whatsapp 0754645826
rashidmsiri@gmail.com



Post a Comment